HAKUNA familia ambayo inaweza kusema haijawahi kula viazi vitamu. Huo ndio ukweli kwa sababu hutumiwa na jamii nyingi kuanzia kifungua kinywa na wengine kufanya mlo wa mchana au jioni.
Wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwa mfano, chakula hiki ni maarufu kutokana na kutumiwa kwa wingi wakati wa futari.
Licha ya sababu hizo, viazi vitamu ni zao la pili la mizizi kuzalishwa kwa wingi nchini likitanguliwa na mihogo. Ni zao linalozalishwa kwa kati na mikoa mingi ikiwamo Iringa, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro. Hata hivyo, mikoa ya kanda ya kati hususan Dodoma na Singida ndio inayoongoza kwa uzalishaji.
Pamoja na kutumiwa zaidi kwa chakula, viazi vitamu ni zao ambalo huchangia kumwondoa mkulima au mdau katika lindi la umaskini. Ushuhuda mkubwa uko kwa wananchi wa wilaya ya Gairo mkoani Morogoro hususan kijiji cha Mtumbatu, barabara kuu ya Morogoro- Dodoma.
Kijiji hicho ni maarufu kwa biashara ya viazi vitamu na ni tegemeo la wengi katika mahitaji ya aina hiyo ya chakula. Watu mbalimbali, wakiwamo watu maarufu kama wanasiasa, wengi husimama sehemu hiyo kwa ajili ya kujipatia mahitaji mbalimbali vikiwamo viazi vitamu.
Biashara ya bidhaa hiyo imebadilisha hata maisha ya wakazi wake kwani kupitia viazi vitamu, baadhi wamefanikiwa kuwa na makazi bora pamoja na kusomesha watoto wao. Hiyo ni simulizi ya baadhi ya wananchi waliokutwa miaka kadhaa iliyopita wakijishughuliha na biashara hiyo kwenye kijiji hicho.
Mbali na kuwapo kwa viazi hivyo ambavyo ndani vina rangi nyeupe au ya maziwa kwa ndani, hivi sasa kumeibuka kilimo cha viazi karoti (vyenye rangi ya karoti kwa ndani) maarufu kama viazi lishe. Baadhi ya watu waliochangamkia kilimo cha jamii hiyo ya viazi ambavyo vina pigiwa debe karibu duniani kote wameelezea ‘siri ya urembo’ iliyomo katika viazi hivyo.
Festo Sebastian, mkulima na mzalishaji wa mbegu za viazi lishe anabainisha kuwa viazi lishe vimebadilisha hali yake ya kimaisha. Kwa maneno mengine, vimesaidia ‘kuupiga teke’ umaskini wa hali na wa kipato.
“Si hivi nilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita. Kwa sasa maisha yangu yamebadilika kwa sababu ya viazi lishe ambavyo navizalisha kwa wingi na vina soko sana baada ya watu kubaini kuwa vina manufaa makubwa kiafya,” alisema Sebastian wakati wa maonyesho ya bidhaa zitokanazo na viazi lishe yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni sambamba na mkutano wa nane wa kimataifa wa kitaalamu wa wanasayansi kwa ajili ya kujadili maendeleo ya kilimo cha viazi lishe kwa kipato na afya.
Aidha, kutokana na umuhimu wa viazi lishe kwa afya na kibiashara, pia kumeibuka makundi ya wasindikaji wa bidhaa mbalimbali kama vile juisi, mikate, keki, tambi maandazi, unga wa lishe ambao unaweza kutumika kwa ugali au uji na ‘crisps’.
UMUHIMU KIAFYA
Kwa upande wa afya, imebainika kuwa viazi lishe vina manufaa makubwa na matumzi yake yanaweza kumfanya mtu kuondokana na maradhi mbalimbali. Kwa mantiki hiyo, utafiti umeonyesha kuwa jamii hiyo ya viazi, vina umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu wakiwamo wanawake na watoto.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Miwa Kibaha, Dk. Kiddo Mtunda, anasema viazi lishe vina manufaa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na kinamama walio katika umri wa kunyonyesha.
“Viazi lishe vina virutubisho kadhaa ambavyo husaidia kuimarisha afya ya binadamu. Kwanza kabisa, vina vitamini A ambavyo husaidia kuimarisha uoni na kumwepusha mtu dhidi ya uoni hafifu au upofu,” anasema huku akiongeza kuwa vitamini A pia ni muhimu kwa afya ya ngozi na kinga dhidi ya maradhi mbalimbali.
Aliongeza kuwa: “Baadhi ya chembe za vitamini A zenye karotini, husaidia kusafisha mwili na ni kinga dhidi ya maradhi na kuzeeka kabla ya wakati.”
Dk. Mtunda pia anabainisha kuwa viazi lishe vina nyuzi nyuzi ambazo husaidia kurahisisha mmeng’enyo wa chakula tumboni, hivyo kuunguza uwezekano wa kansa ya utumbo mkubwa.
Maneno hayo ya Dk. Mtunda, yalitiwa uzito na Dk. Richard Kasuga, Mratibu Mwandamizi wa Kituo cha Kimataifa cha Viazi kwa Tanzania ambaye alisema: “Viazi lishe vina umuhimu mkubwa kwa sababu vinasaidia ukuaji wa watoto na kuondoa tatizo la udumavu, kuimarisha afya ya uzazi na matatizo ya vitamini A.”
Naye Domina Nkuba, Mtafiti Lishe kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Mikocheni (MARI), Dar es Salaam anasema jamii hiyo ya viazi viko katika makundi ya vyakula vya wanga, protini, vitamin, madini, mafuta na sukari.
“Kwa mantiki hiyo, viazi lishe vina wanga, vitamini na madini ambavyo matumizi yake yana manufaa makubwa kiafya. Licha ya kuimarisha afya, ni muhimu katika kupunguza utapiamlo, kupambana na upungufu wa vitamini A kwa wajawazito, watoto na wazazi,” alisema.
Kutokana na umuhimu huo, Nkuba alisema iwapo kila mjamzito atatumia viazi lishe, kinga ya mwili itaimarika na kusababisha kupungua kwa vifo vya uzazi kwa sababu mama atakuwa na afya imara na wakati huo huo, mtoto aliyeko tumboni atakuwa na afya nzuri.
KINGA MAGONJWA SUGU
Pamoja na faida mbalimbali kiafya zitokanazo na viazi lishe au viazi karoti kama inavyojulikana sehemu zingine, imebainika kuwa ni kinga na ina manufaa makubwa katika kupambana na maradhi sugu kama vile saratani, kisukari na yale nyemelezi kama malaria kwa mtu mwenye virusi vya Ukimwi (VVU).
Nkuba alisema ulaji wa viazi lishe humkinga mtumiaji dhidi ya uwezekano wa kupatwa ma maradhi ya kansa hasa tezi dume na ile ya mlango wa kizazi pamoja na saratani ya utumbo mpana.
Nkuba pia alisema utafiti uliofanywa na wataalamu wa masuala ya lishe na afya unaonyesha kuwa viazi lishe, kutokana na kuwa na karotini nyingi ndani yake, husaidia kurekebisha kiwango cha sukari kwenye damu.
Aidha, utafiti unaonyesha kuwa kutokana na viazi hivyo kuwa na vitamini A kwa wingi, watoto wanapotumia huwa katika nafasi nzuri ya kukingwa na maradhi mbalimbali kama surua, kuharisha, upofu, vichomi na vitamini hizo zinapokosekana mwilini, mwili wa mtoto unakuwa katika hatari ya kushambuliwa na maradhi kirahisi.
“Mtu mzima anapokosa vitamini A, mwili wake unaweza kukosa au kupungua kinga na hivyo kuwa rahisi kupata magonjwa na wakati mwingine kuchelewa kupona,” unabainisha utafiti huo.
HALI HALISI
Ukosefu wa vitamini A bado ni changamoto nchini hasa kwa wanawake walio katika umri wa kunyonyesha ambao ni kuanzia miaka 15 hadi 49 na watoto walio chini ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Nkuba na Nyamizi Bundala mwaka 2016, ukosefu wa lishe bora umesababisha watoto chini ya umri wa miaka mitano kuwa na tatizo kubwa la kiafya.
Kutokana na ukosefu huo, asilimia 42 ya watoto wanakabiliwa na tatizo la udumavu na asilimia 16 uzito mdogo huku asilimia 59 wakiwa na upungufu wa damu. Aidha, asilimia 33 wana ukosefu wa vitamini A.
Wanawake wenye umri kati ya miaka 15 na 49, kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 11 wana tatizo la ukondefu, 40 wana upungufu wa damu na asilimia 37 wana ukosefu wa vitamini A.
Akifungua mkutano wa nane wa kimataifa wa kitaalamu wa wanasayansi kujadili maendeleo ya kilimo cha viazi lishe kwa kipato na afya jijini Dar es Salaam jana, Septemba 25, mwaka huu, Mkurugernzi wa Utafiti na Maendeleo kutoka Wizara ya Kilimo, Dk. Hussein Mansour, alisema ukosefu wa vitamini A unachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya wanawake wakiwamo wajawazito.
Pia alisema watoto pia wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na ukosefu wa vitamini hizo hivyo kuwa na udumavu unaosababisha ukuaji wa mwili na ubongo kuwa hafifu, hivyo jitihada zaidi zinatakiwa ikiwamo suala la lishe kupewa kipaumbele kwa maendeleo ya taifa.
“Utafiti uliofanyika mwaka 2016 umeonyesha hali bado ni mbaya na hii inatokana na ukweli kwamba asilimia tisa tu ya watoto wenye umri wa miezi sita hadi 23 ndio wanaopata kiwango cha chini cha chakula kinachotakiwa,” alisema.
Dk. Mansour alisema sababu ya tatizo hilo kuwa kubwa ni kutokana na watu kuacha kutumia vyakula vya asili ambavyo vina vitamini zinazotakiwa na kukimbilia vile vinavyotengenezwa viwandani.
“Vyakula hivi vya kutengenezwa viwandani vinauzwa kwa bei kubwa ambayo watu wa vijijini wengi wao hawawezi kununua…jitihada pia zinapaswa kufanyika kwa kutoa elimu ya kilimo bora cha viazi lishe ambavyo nina madini mengi ya vitamini A ambavyo pia vinaweza kuwaondoa watu katika umaskini walio nao.
Naye Meneja wa Kituo cha Kimataifa cha Viazi Vitamu (CIP) Uganda, Robert Mwanga, alisema tatizo la upungufu wa Vitamin A kwa nchi za Afrika ni kubwa na utafiti uliofanyika na taasisi hiyo unaonyesha athari kubwa iko kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.
Alisema katika utafiti huo, wanawake wenye umri wa kuzaa na wanaonyonyesha, wenye tatizo hilo nchini Uganda ni asilimia 33 huku nchi zingine zikiwa na kiwango cha takriban asilimia 50.
“Hili ni tatizo kubwa kwa Afrika na nchi zinazoendelea kwani ukiangalia nchi zilizoendelea si kubwa kama kwetu (Afrika). Marekani ni asilimia mbili tu na wanaoathirika ni wageni wanaoingia nchini humo,” alisema.
Alisema kutokana na tatizo hilo kuendelea kuwa kubwa na kusababisha athari, mkutano huo wa wadau kutoka nchi 17 na taasisi mbalimbali za utafiti na lishe, umekusudia kulizungumzia kwa kina na kuweka mikakati ya kupunguza.
Thanks for reading Maajabu ya viazi lishe kwa afya
Comments
Post a Comment