ULAJI UNAOFAA NA MTINDO BORA WA MAISHA


Karibu kwenye blog ya AFYA YAKO ni matumaini yangu umzima wa afyanatumshukuru mungu kwa kuendelea kutuazima pumzi. Leo tutaangalia ULAJI UNAOFAA.
ULAJI UNAOFAA ni nini?
Ulaji unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko, cha kukutosha kukua na kuwa na uzito wa kawaida na chenye virutubishi vyote kwa uwiano unaotakiwa.
Kula matunda angalau mara mbili kwa siku, kula mbogamboga kwa wingi, tumia mafuta kwa kiasi kidogo (pendelea zaidi mafuta yatokanayo na mimea) na tumia sukari na chumvi kwa kiasi kidogo.

KULA MLO KAMILI WENYE CHAKULA MCHANGANYIKO.
Chakula chenye mchanganyiko hukuwezesha kupata virutubishi vyote vinavyohitajika mwilini.

  • Mfano vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto, Protini husaidia kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali, Vitamini na Madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa.
  • Virutubishi kwenye kila aina ya chakula hutofautiana, na virutubishi hutegemeana ili kufanya kazi kwa ufanisi.
  • Kila siku jitahidi kula vyakula kutoka kila mojawapo ya makundi yafuatayo;







  1. VYAKULA VYENYE ASILI YA NAFAKA - Mahindi, Mtama, Ulezi, Mchele, Mihogo, Viazi vikuu, Viazi vitamu, Magimbi, Ngano na Ndizi za kupika.
  2. VYAKULA VYA JAMII YA KUNDE NA VYA ASILI YA WANYAMA - Maharagwe, Njegere, Karanga, Mbaazi, Kunde, Nyama, Mayai, Maziwa, Samaki, Dagaa, Kuku na Wadudu wanaoliwa kama vile Senene na Kumbikumbi.
  3. MATUNDA - Embe, Peasi, Zeituni,Fenesi, Ndizi mbivu, Papai, Pera, Chungwa, Ubuyu, Nanasi, Pesheni, Parachichi na Zambarau.
  4. MBOGAMBOGA - Mchicha, Majani ya Maboga, Kisamvu, Majani ya kunde, Matembele, Spinachi, Mnavu, Mchunga, Kabichi, Bamia, Karoti, Biringanya, Nyanya, Matango, Mlenda, Boga, Nyanya Chungu.
  5. MAFUTA - Mafuta ya Alizeti, Mafuta ya Nazi, Mafuta ya Mawese, Ufuta, Mafuta ya Karanga, Mafuta ya Majarini na Siagi.


  • Maji hayahesabiwi kama kundi la chakula lakini ni muhimu sana kwa kurekebisha joto la mwili na kuondoa mabaki/uchafu mwilini kwa njia ya jasho na mkojo.
KUTOKULA MAFUTA MENGI

  • Mafuta ni muhimu mwilini lakini yanahitajika kwa kiasi kidogo tu.
  • Mafuta mengi mwilini hasa yale yenye asili ya wanyama yanaweza kusababisha ongezeko la magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
  • Inashauriwa kutumia zaidi mafuta yatokanayo na mimea ambayo huwa kwenye hali ya kimiminika katika joto la kawaida na hivyo si rahisi kuganda kwenye mishipa ya damu.
  • Jinsi ya kupunguza mafuta:
  1. Tumia mafuta kidogo wakati wa kupika.
  2. Punguza mafuta kwenye nyama iliyonona, na ikibidi ondoa ngozi kabla ya kuipika.
  3. Chagua nyama au samaki wasio na mafuta mengi.
  4. Epuka vyakula vilivyokaangwa au kupikwa kwa mafuta mengi - Sambusa, Chipsi n.k. Badala yake pendelea vyakula vilivyochemshwa au kuchomwa.
KULA MATUNDA NA MBOGAMBOGA KWA WINGI
  • Vyakula hivi huupatia mwili kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na kuupatia makapi-mlo(fibre au rouphage) ambayo humfanya mtu ajisikie kushiba na kupunguza kiasi cha chakula anachokula na hivyo kupunguza uwezekano wa kuwa na uzito uliozidi.
  • Matunda ni chanzo cha virutubisho/viinilishe vya vitamini na madini ambayo hupatikana kwa wingi kwenye vyakula hivi kuliko kwenye vyakula vingine.
  • Virutubisho hivi:
  1. Hufanya ngozi kuwa ng'aavu na yenye afya na vidonda kupona vizuri.
  2. Huwezesha macho kuona vizuri.
  3. Husaidia kuimarisha ufahamu.
  4. Husaidia uyeyushaji wa vyakula tumboni na kufyonza madini mwilini.
  5. Hutumika katika kutengeneza damu.
  6. Husaidia katika uundaji wa chembe za uzazi.
  • Virutubisho hivi havihifadhiki katika mwili wa binadamu hivyo ni vizuri matunda tofauti yajumlishwe kwenye milo ya kila siku.
  • Pika mbogamboga kwa muda mfupi ili kupunguza upotevu wa vitamini na madini.
  • Tumia maji kidogo wakati wa kupika mbogamboga. Maji yanayopikia mbogamboga yaendelee kutumika sio kumwagwa.
VYAKULA VYENYE NYUZINYUZI (makapi-mlo).
Vyakula vyenye nyuzi nyuzi husaidia katika usagaji wa chakula tumboni na pia huweza kupunguza baadhi ya saratani, magonjwa ya moyo na kisukari. Ili kuongeza nyuzinyuzi
  • Kula matunda na mbogamboga mara kwa mara.
  • Kula tunda zima badala ya Juisi.
  • Tumia unga wa nafaka zisizokobolewa (Dona, atta, n.k)
  • Kula vyakula  vya jamii ya kunde mara kwa mara kwani zina nyuzinyuzi kwa wingi.
PUNGUZA CHUMVI
  • Chumvi isizidi gramu tano (kijiko kidogo cha chai) kwa mtu mmoja kwa siku.
  • Tumia chumvi kidogo wakati wa kupika
  • Jenga tabia ya kutoongeza chumvi ya ziada mezani wakati wa kula.
  • Epuka vyakula vilivyosindikwa au vyenye chumvi nyingi kama vile soseji n.k
PUNGUZA SUKARI
  • Kunywa vinywaji ambavyo havina sukari kam vile madafu na juisi halisi za matunda.
  • Kama unatumia sukari tumia kwa kiasi kidogo.
  • Punguza vitu vyenye sukari nyingi nyingi kama vile soda, juisi za viwandani, keki, pipi, chokoleti, jamu n.k
  • Punguza matumizi ya vya vyakula vilivyoongezwa sukari.
MWISHO
Huo ndio mwisho wa somo letu kwa leo lililokuwa linazungumzia ULAJI UNAOFAA NA MTINDO BORA WA MAISHA katika kipengele cha ULAJI UNAOFAA. Tukutane wakati mwingine kwenye kipengele kinachofuata cha ULAJI BORA KWA MAKUNDI MBALIMBALI KATIKA JAMII.
Usisahau ku like, ku comment na ku share kwa wengine zaidi
CHAOOOOOO😍😍😍 

Comments