Utakubaliana na mimi kwamba, kitendo cha mtu kubanwa na haja ndogo siyo
kitu cha hiyari kwamba sasa mtu anaamua ngoja nibanwe na mkojo, hili ni
jambo la asili na ni matokeo ya vyakula, matunda au vinywaji
tunavyotumia. Kwa lugha nyingine tumekuwa tukiita kuwa ni wito wa asili
au nature’s call.
Yawezekana mtu akawa katika mkutano, safarini, akawa katika mitandao ya
kijamii anachati au popote pale akiwa anafanya jambo fulani na kutokana
na jambo hilo, mtu akaendelea kujibana na kutokwenda kuyapunguza maji
haya kutoka katika kibofu cha mkojo kwa kutoa kipaumbele kwa shughuli
anayoifanya kuliko kusikiliza kwanza wito huu wa asili. Mambo haya
tunayafanya sana, utasikia, mkojo umenibana kweli, ila ngoja nimalizie
hii kazi halafu niende kujisaidia, hivi ndivyo watu wengi wanafanya.
Kutokana na vyakula na vinywaji tunavyotumia, kibofu cha mkojo
huanza kujaa mkojo, mkojo unapofikia karibu mililita 50 mpaka 500 mtu
huanza kuhisi hitaji la kwenda kukojoa. Kibofu cha mkojo kimezungukwa na
vigunduzi asili (Receptors) vinavyopeleka taarifa katika Ubongo
kuonyesha kuwa kibofu cha mkojo kimekaribia au kimejaa, baada ya taarifa
hizi kufika katika ubongo, ubongo unatoa taarifa katika kibofu cha
mkojo ili kiweze kushikilia mkojo huo kwa kuikaza misuli maalumu
(Sphincters) mpaka hapo muda wa wewe kwenda kukojoa utakapofika.
Kibofu
cha mkojo hufanya kazi kwa mfumo wa kujiendesha wenyewe yaani,
automatic, kitendo cha mtu kupuuzia kwenda kukojoa husababisha Ubongo
upate usumbufu wa taarifa za kujaa kwa kibofu cha mkojo na kwa kuwa
Ubongo nao hutuma taarifa katika kibofu cha mkojo kusema kuwa mkojo
uendelee kushikiliwa mpaka muda muafaka utakapofika, itafika kipindi
uwezo wa ubongo kutoa taarifa hizi na pia uwezo wa vigunduzi asili
(Receptors) vilivyoko katika kibofu cha mkojo kupoteza uwezo wake tena
wa kufanya kazi hizo au uwezo kuwa mdogo. Matokeo yake ni mtu siku kweli
anahitajika kuvumilia kidogo ili afike sehemu inayostahihi kujisaidia,
lakini hawezi tena na kujikuta muda mdogo tu….mtu tayari kaloanisha nguo
yake.
Mpenzi msomaji, mtu kujibana na kupuuzia kwenda kukojoa
husababisha uwezo wa kibofu cha mkojo kujitawala (control) upotee. Pia
kama uwezo wa neva zinazopeleka taarifa kwenye ubongo kuhusu
mabadiliko/ujazo wa kibofu cha mkojo zitaharibika, basi misuli maalumu
ya kubana mkojo (sphincter) itashindwa kuachia na matokeo yake mtu
ataendelea kukaa na mkojo katika kibofu chake kwa muda mwingi zaidi kitu
ambacho ni hatari kwa afya yake. Endapo mkojo huu utashindwa kutoka,
utatengeneza mazalia ya bakteria na kukusababishia magonjwa ya kibofu
(bladder infection). Magonjwa ya kibofu cha mkojo ni pamoja na U.T.I
(Urinary Tract Infections), pia huweza kusababisha magonjwa ya figo na
mchafuko wa damu, bacteremia.
Kuna hali huwa inajitokeza kwa
baadhi ya watu, yawezekana alikuwa kabanwa na mkojo au alikuwa hajahisi
kwenda kukojoa, ila akinywa maji au akisikia sauti ya maji yanachuluzika
mfano maji yakitoka bombani, basi atahisi kwenda kukojoa.
Mpenzi
msomaji, ni vyema tukawa wasikivu pale mtu unapobanwa na mkojo, hii ni
kwa ajili ya afya ya kibofu chako cha mkojo lakini pia ni kwa ajili ya
afya yako kwa ujumla. Kama unalo tatizo, usisite kuonana na wataalamu wa
afya.
#AFYAYAKO UPDATES
Comments
Post a Comment