MADHARA YA KULA CHUMVI NYINGI

 


CHUMVI ni moja ya vitu vilivyomo katika maji ya baharini, baada ya maji kuwa mvuke baada ya kupata joto, chumvi hubaki kama vichangarawe vidogovidogo ambavyo huvunwa na kutumika kama kiungo.

Ukipita majumbani, hoteli zote, migahawa, minadani, matamasha na mitaani vijiwe vya nyama choma utashuhudia ulaji mkubwa wa chumvi. Watu hujimiminia chumvi katika chakula hata kama chakula hicho kina chumvi.

Wengi wao hawafahamu kama ulaji chumvi kwa mtindo huo ni hatari kwa afya zao. Chumvi ni muhimu sana kwa mwili wa mwanadamu kwa kuwa huwa na kiambata kiitwacho sodium ambacho ni muhimu kwa kazi za kimwili.

Chumvi imebeba sodium chloride, ndani yake takriban asilimia 40 kati ya hizo ni sodium. Mfumo wa fahamu hutumia sodium kwa ajili ya mipitisho mbalimbali, ukunjikaji au kujivuta kwa misuli, udhibiti wa kiwango sahihi cha maji na uwiano sahihi wa chumvichumvi mwilini hutegemea sodium.

Mwili hutumia sodium kwa ajili ya kudhibiti wingi wa maji katika damu, ogani na tishu za mwilini pale inapozidi, basi figo huwa na kazi ya kuitoa kwa njia ya mkojo. Ingawa kama utakula kwa kiasi kingi, basi figo hushindwa kutoa kiasi chote hivyo huendelea kubaki mwilini ndipo matatizo mbalimbali hujitokeza.

Madhara ya chumvi kiafya ni kama vile kupata shinikizo la damu. Msukumo wa damu mwilini hutegemea na uwepo wa sodium. Pale sodium inapokuwa imezidi mwilini, msukumo wa damu nao unakuwa juu na hatari. Uwepo zaidi wa sodium ni pale mhusika anapokuwa tayari ana shinikizo la damu, ugonjwa ambao huwa hauonyeshi dalili mwanzoni.

Mgonjwa hugundulika pale anapokuwa anapata matibabu mengine hospitalini. Kiasi cha damu katika mzunguko ni moja ya vitu vinavyosababisha uwepo wa msukumo wa damu mwilini.

Pale utakapokula kiasi kikubwa cha chumvi zaidi ya uwezo wa figo zako kuhimili kiasi kilichozidi cha chumvi mwilini hubaki, kutokana na tabia ya sodium kuvuta maji kiasi kilichozidi kitabakiza maji mengi mwilini na hivyo ujazo wa damu utaongezeka katika mzunguko na hivyo shinikizo la damu hutokea.

Vilevile, sodium iliyopo kwenye chumvi hutegemewa na seli za misuli ya moyo ili kuongeza mapigo, pale inapozidi mapigo huwa juu na hivyo shinikizo la damu hutokea. Ndiyo maana huwashauri wagonjwa wenye shinikizo la damu kupunguza sana chumvi kwenye chakula hasa ya kuongeza.

Kula chumvi nyingi kunasababisha magonjwa mengine ya moyo na kiharusi (stroke). Kama msukumo wa damu utakuwa mkubwa zaidi inaweza ikasababisha mishipa yako ya damu ikawa inashindwa kutanuka na kukuweka katika hatari ya kujengeka kwa mrundikano wa mafuta kitaalamu huitwa plaque.

Hali hiyo inasababisha tatizo katika mishipa ya damu kitaalamu huitwa atherosclerosis. Tatizo hili ni hali ya mishipa kuwa migumu. Mishipa ya ateri huweza kuharibika na kuwa myembamba au kusinyaa na kuta za mishipa hiyo hukakamaa.

Hali hii huufanya moyo kuwa na kazi ngumu na hivyo inakuweka katika hatari ya kupata shambulizi la moyo la ghafla, moyo kushindwa kufanya kazi na kusababisha kiharusi. Tafiti za shule ya afya ya jamii ya Harvard, Marekani inaonyesha utumiaji chumvi kupita kiasi unaongeza asilimia 23 ya kuweza kupata kiharusi na asilimia 14 kupata magonjwa ya moyo.

Matatizo mengine ni kama vile moyo kuwa mkubwa na valvu kuwa na matatizo, kwani uwepo wa ujazo mkubwa wa chumvi katika mzunguko wa damu inamaanisha moyo kufanya kazi ya ziada ili kuleta mzunguko sahihi unaotakiwa na mwili. Chumvi husababisha magonjwa mengine kama ya figo, mwili kuvimba na upungufu wa maji, tindikali kuwa nyingi tumboni, udhaifu wa mifupa, vichochezi na chumvi chumvi katika mwili kutowiana.

USHAURI

Moja ya nyenzo kuu za kupambana na tatizo hili ni kubadili mienendo na mifumo ya kimaisha kwa kuhakikisha tunaepuka ulaji vyakula vyenye chumvi hasa ya kuongeza mezani, kunywa maji mengi, kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara.

 Thanks for reading Madhara ya kula chumvi nyingi

Comments