KENYA: WATOTO 4,000 WAPACHIKWA MIMBA MACHAKOSI

Takwimu hizo zilifichuliwa na Afisa wa watoto wa Kaunti ya Machakos, Bi Salome Muthama ambaye alisema kati ya Januari na Mei mwaka huu, ilibainika kuwa wasichana 3,964 wenye umri mdogo walishika mimba.

“Wazazi wametelekeza majukumu yao. Hawazungumzi na watoto wao, ambao mwishowe hujifunza mambo ya kupotosha katika mitandao ya kijamii na sehemu nyingine zisizostahili,” akasema.

Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua (pichani, ukurasa wa kwanza) alisema ingawa wakati mwingi visa aina hii husemekana kusababishwa na wanaume wakomavu wanaohadaa wasichana, watoto wamekuwa wakishiriki ngono wenyewe kwa wenyewe.

“Lazima tukubali kuwa ingawa kuna watu wazima wanaonyemelea watoto, kuna wavulana ambao ni marika ya hawa wasichana wanaoshiriki ngono. Wanaume wanaonajisi watoto wetu wanafaa kuadhibiwa lakini pia tuzungumze na watoto wetu wa kiume,” akasema gavana huyo.

Kaunti-ndogo ya Masinga inaongoza kwa visa 601 vya wasichana waliopata mimba wakiwa na umri wa kati ya miaka 15 na16.

Kaunti-ndogo ya Athi River ilikuwa ya pili ikiwa na visa 561 vya wasichana wa umri wa kati ya miaka 15 na 19 waliopata mimba katika kipindi hicho.

Takwimu zinaonyesha kuwa eneo la Mwala lilikuwa na wachana 526 waliotungwa mimba wakiwa na umri wa kati ya miaka 15 na 19 na sita waliokuwa na umri wa kati ya miaka 10 na 14.

Kaunti-ndogo ya Machakos Mjini ilikuwa na wasichana 259 waliopachikwa mimba wakiwa na umri wa miaka 15-19 na 48 wakiwa na umri wa 10-14.

Matungulu ilisajili wasichana 506, Kalama (148), Kangundo (323), Kathiani (403) na Yatta (34).

Bi Muthama alisema kwamba iwapo hatua hazitachukuliwa maisha ya baadaye ya wasichana katika kaunti hiyo yamo hatarini.

Alizidi kusema kuwa inashukiwa kuna visa vingi ambavyo havijaripotiwa. Alikuwa akihutubia wanahabari siku ya kuadhimisha siku ya mtoto Mwafrika mnamo Jumanne katika makao ya watoto ya Machakos Rescue Centre.

Idadi hiyo iligutusha Wakenya wengi waliokadiria kuwa iwapo kaunti moja inaweza kurekodi visa vipatavyo 4,000 kwa muda mfupi kama huo, basi kitaifa huenda idadi hiyo ikafika laki kadhaa hasa inapozingatiwa kuwa kuna kaunti ambazo mimba za mapema zimekithiri kuliko Machakos.
#AfyayakoUPDATES

Comments