Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa amezielekeza FCC,
EWURA, WMA kufanya ukaguzi na kuwachukulia hatua wafanyabiashara na
waagizaji wa mafuta wanaoficha bidhaa hiyo kwa lengo la kuyauza kwa bei
ya juu yatakapoadimika au kupanda bei.
Waziri Bashungwa aliyasema Juni 17, 2020 jijini Dar es salaam katika
kikao kazi na Watendaji wa Mamlaka za Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Vipimo (WMA), Mamlaka
ya Bandari (TPA) pamoja na TRA kwa lengo la kufanya mapitio na
marekebisho ya utaratibu wa kanuni ya bei elekezi ya mafuta kwa bidhaa
za petroli zinazoingizwa nchini kupitia bandari za Dar es Salaam, Mtwara
na Tanga, kwa nia ya kuwezesha manufaa ya punguzo la bei kuwafikia
wananchi sa mikoa yote nchini kwa usawa.
‘‘Katika kipindi cha mapambano ya Covid-19, moja ya fursa tulizozipata
kama nchi ambayo pia tulipata maambukizi ni kushuka kwa bei ya mafuta,
na sisi kwa sababu tunaingiza mafuta kutoka nje ya nchi, kushuka kwa bei
ya mafuta duniani sisi tumenufaika lakini pamoja na kunufaika huku kwa
kushuka kwa bei ya mafuta kuna baadhi ya mikoa bado bei ipo juu”
Aidha, Bashungwa ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wote ambao bado
wana tabia za kuficha bidhaa mbalimbali pindi zinaposhuka bei au
kuadimika kwa lengo la kujipatia kipato kikubwa, ameielekeza taasisi ya
Tume ya Ushindani na Ewura kufanya msako mkali kama ulifanywa kwenye
sukari ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote
wanaoendeleza tabia hizo
"Wafanyabiashara tunajua bei ambazo wananunulia mafuta na kipindi cha
COVID-19, mfanyabiashara yoyote ambaye amenunua mafuta kwa bei ya
punguzo lakini punguzo hilo halijaenda moja kwa moja kwa mlaji kwa maana
ya mwananchi maeneo yote nchini ambayo wafanyabiashara hawa wanaingiza
mafuta na kusambaza, tutatumia taasisi zetu ya Tume ya Ushindani na
Ewura kuhakikisha kote nchini tunafatilia na kama kuna mfanyabiashara
yoyote wa mafuta ambaye ana hodhi mafuta ili kupata faida tutatumia
sheria kumchukukulia hatua kali kama tulivyofanya kwenye sukari,"
Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa kuwa mapendekezo ya wataalamu katika
kikao kazi hicho yatapelekwa kwa Waziri mwenye dhamana ya Nishati na
Madini baada ya kukamilika leo hii ili kumshauri kuhusu namna ya kuweka
uwiano sawa wa bei elekezi kwa bidhaa husika, huku akisisitiza kuwa
wafanyabiashara watakaobainika kukiuka taratibu za leseni walizopatiwa
na EWURA na wanaokiuka kanuni, sheria na taratibu za Ushindani
watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kunyang'anywa leseni za kufanya
biashara ya bidhaa za petrol
Awali, Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(EWURA), Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema kuwa “Mafuta yanayouzwa
nchini yanapokelewa kupitia bandari za Dar es salaam, Tanga na Mtwara.
Katika kukokotoa bei ya mafuta, mikoa ya Kaskazinini (Tanga,
Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hupangiwa bei zao kulingana na gharama
ya mafuta yanayopokelewa kupitia bandari ya Tanga. Mikoa ya kusini
(Mtwara, Lindi na Ruvuma) hupangiwa bei kulingana na gharamaya mafuta
yanayopokelewa kupitia bandari ya Mtwara. Mikoa mingine yote hupangiwa
bei zao kulingana na gharama ya mafuta yaliyopokelewa kupitia bandari ya
Dar es salaam.
Sambamba na hayo Mhandisi Godfrey amesoma mapendekezo ambayo yataleta mabadiliko ya kanuni za kukokotoa bei za mafuta ambayo ni;
Kuweka usawa wa premium kwa bandari zote na hivyo kuwa na bei za mafuta
zenye ushindani na watumiaji wa mafuta kununua kwa bei ambayo ina usawa,
kuweka kanuni za kubadilisha gharama za mafuta kila mwezi kulingana na
mabadiliko ya soko la dunia, kuendelea kuwepo kwa nafasi ya ushiriki wa
kampuni za wazawa katika zabuni za BPS.
#AfyayakoUPDATES
Comments
Post a Comment