RWANDA YARIPOTI KIFO CHA KWANZA CHA MGONJWA WA KORONA

Rwanda

Wizara ya Afya nchini Rwanda imeripoti kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona aliyetajwa kuwa ni dereva wa malori mwenye umri wa miaka 65.

Taarifa ya Wizara hiyo iliyotolewa jana imeeleza kuwa mgonjwa huyo alipata maambukizi akiwa nchi jirani alikoenda kikazi, lakini alipozidiwa aliamua kurejea nchini humo kwa ajili ya matibabu. Mgonjwa huyo alipatiwa matibabu kutoka kwa wataalam wa afya lakini alifariki kutokana na matatizo ya kupumua.

Hadi jana, Mei 30, 2020, visa vya corona vilifikia 359 nchini Rwanda, lakini wagonjwa 250 kati ya hao walishapona na wameruhusiwa kutoka hospitalini. Wagonjwa wanaendelea kupatiwa matibabu hadi sasa ni 108, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya.

Rwanda imelegeza masharti ya kubaki nyumbani (lockdown), na imeruhusu baadhi ya biashara kufunguliwa baada ya kufungwa kwa muda kama hatua za awali za kuchukua tahadhari.

Inatarajiwa kuwa kesho, Juni 1, 2020 waendesha pikipiki (bodaboda) wataanza kuruhusiwa kubeba abiria pamoja na kuruhusu mizunguko mingine ya utafutaji riziki baada ya kufungwa kwa takribani miezi miwili.

Wananchi wameendelea kupewa elimu na kutakiwa kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya kujikinga na virusi vya corona, kwani virusi hivyo bado vipo.

Comments