ZINGATIA LISHE BORA
Kula vyakula vya aina mbalimbali
Ukiwa mjamzito au unayenyonyesha mwili wako unahitajimlo kamili unaotokana na vyakula vya aina mbalimbali. kula vyakula mbalimbali kila siku husaidia kuhakikisha kuwa unapata nguvu na virutubishi vyote unavyohitaji wewe na mtoto wako.
Lishe bora husaidia
- Kuongeza uzito angalau kilo 12 wakati wa ujauzito kwa wastani wa kilo 1 kila mwezi.
- Kuzuia upungufu wa damu.
- Kuboresha ukuaji wa mtoto wako kimwili na kiakili.
- Kuutayarisha mwili kwa ajili ya kunyonyesha. Mahitaji ya chakula na virutubishi ni makubwa unaponyonyesha kuliko ukiwa mjamzito.
- Kupunguza uwezekano wa kupata mtoto mwenye uzito pungufu, kujifungua kabla ya wakati au kupata mtoto mfu.
KULA MLO KAMILI.
Jinsi ya kupanga mlo kamili
Kula walau milo mitatu iliyo kamili na asusa (vitafunwa) kila siku. Chagua vyakula kutoka kila kundi katika makundi yafuatayo:
1. VYAKULA VYA NAFAKA
Kwa mfano: mahindi, mtama, mchele, ulezi, ngano, muhogo, ndizi za kupika, viazi vitamu, viazi vikuu na magimbi.
2. VYAKULA VYA JAMII YA KUNDE NA VYA ASILI YA WANYAMA
Kwa mfano: maharage, njegere, karanga, mbaazi, kunde, nyama, mayai, maziwa, samaki, dagaa, kuku, na wadudu wanaoliwa kama senene na kumbikumbi.
3. MATUNDA
Kwa mfano: embe, ndizi mbivu, papai, pera, chungwa, ubuyu, nanasi, pesheni, parachichi na zambarau.
4. MBOGAMBOGA
Kwa mfano: mchicha, majani ya maboga, kisamvu, matembele, bamia, karoti, nyanya chungu, nyanya, matango, mlenda, boga na biringanya.
5. MAFUTA.
Kwa mfano: mafuta ya alizeti, nazi, mawese, mbegu zinazotoa mafuta, majarini na siagi.
Mafuta yakiongezwa kwenye mbogamboga na vyakula vingine huboresha ufyonzaji wa baadhi ya vitamini na huongeza nguvu mwilini.
LINDA AFYA YAKO
Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanahitaji
- Kula chakula kingi katika kila mlo au kula milo midogomidogo mara nyingi.
- Kula asusa kati ya mlo na mlo.
- kunywa maji ya kutosha kila siku (glasi 8 au lita 1.5).
- kula matunda na mbogamboga kwa wingi katika kila mlo.
- kuepuka kunywa chai au kahawa pamoja na mlo kwani huzuia ufyonzaji wa madini ya chuma na huweza kusababisha upungufu wa damu. Ni vyema kunywa chai au kahawa saa moja kabla au baada ya kula.
- Kipindi chote cha ujauzito, hadi miezi 3 baada ya kujifungua unahitaji vidonge vya madini ya chuma na vya foliki asidi kuzuia upungufu wa damu. Ni vyema kumeza vidonge vya madini ya chuma pamoja na chakula ili kuongeza ufyonzaji na kupunguza maudhi madogo madogo, hasa kichefuchefu.
- Kila mara tumia chumvi yenye madini joto kuzuia upungufu wa madini joto mwilini.
- Kunywa matone ya Vitamin A mara baada ya kujifungua au ndani ya kipindi cha wiki 6 za kujifungua kama utakavyoshauriwa na mtoa huduma. Hii itasaidia kujenga kinga ya mwili wa mtoto wako.
- Kila mara nawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka kabla ya kutayarisha na kula chakula.
- Weka vyombo na sehemu ya kutayarishia chakula katika hali ya usafi.
- Pika nyama, samaki na mayai mpaka viive kabisa ili kuepuka maambukizo.
- Osha mbogamboga kabla ya kuzikatakata, zipikwe mara moja kwa muda mfupi na kuliwa mara baada ya kupika ili kuhifadhi virutubishi.
- Osha vizuri matunda na mbogamboga zinazoliwa bila kupikwa.
- Anza kuhuduria kliniki ya wajawazito mara tu unapogundua kuwa mjamzito.
- Hudhuria maudhurio yote nane mapaka utakapojifungua ili kufuatilia afya yako na ukuaji wa mtoto wako.
- Usitumie pombe, dawa za kulevya au bidhaa zenye tumbaku.
- Tumia vidonge vya kutibu minyoo ili kuzuia upungufu wa damu.
- Pumzika mchana hasa miezi 3 ya mwisho ya ujauzito na miezi ya mwanzo baada ya kujifungua.
- Tumia dawa za kuzuia malaria na chandarua kilichowekwa dawa ili kuzuia malaria na upungufu wa damu.
- Ni vyema kusubiri miaka 3 baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine ili kuwezesha mwili kurudi kwenye afya nzuri.
MWSHO.
Huo ni mwisho wa somo hili la LISHE wakati wa ujauzito na kunyonyesha, tukutane tena katika masomo mengine.
ASANTENI SANA
😍😍😍😍😍😍
Comments
Post a Comment